Swahili
Sorah As-Saaffat ( Those Ranges in Ranks )
Verses Number 182
Naapa kwa wanao jipanga kwa safu.
Na kwa wenye kukataza mabaya.
Na kwa wenye kusoma Ukumbusho.
Hakika Mungu wenu bila ya shaka ni Mmoja.
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na yaliyomo kati yao, na ni Mola Mlezi wa mashariki zote.
Hakika Sisi tumeipamba mbingu ya karibu kwa pambo la nyota.
Na kulinda na kila shet'ani a'si.
Wasiweze kuwasikiliza viumbe watukufu. Na wanafukuzwa huko kila upande.
Wakifurushwa. Na wanayo adhabu ya kudumu.
Isipo kuwa anaye nyakua kitu kidogo, na mara humfwatia kimondo kinacho ng'ara.
Hebu waulize: Je! Wao ni wenye umbo gumu zaidi au hao wengine tulio waumba. Hakika Sisi tuliwaumba wao kwa udongo unao nata.
Bali unastaajabu, na wao wanafanya maskhara.
Na wanapo kumbushwa hawakumbuki.
Na wanapo ona Ishara, wanafanya maskhara.
Na husema: Haya si chochote ila ni uchawi tu ulio dhaahiri.
Ati tukisha kufa na tukawa udongo na mifupa ndio kweli tutafufuliwa?
Hata baba zetu wa zamani?
Sema: Naam! Hali nanyi ni madhalili.
Huko utapigwa ukelele mmoja tu! Na hapo ndio wataona!
Watasema: Ole wetu! Hii ndiyo Siku ya Malipo.
Hii ndiyo Siku ya Hukumu mliyo kuwa mkiikadhibisha.
Wakusanyeni walio dhulumu, na wake zao, na hao walio kuwa wakiwaabudu -
Badala ya Mwenyezi Mungu. Waongozeni njia ya Jahannamu!
Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa:
Mna nini? Mbona hamsaidiani?
Bali hii leo, watasalimu amri.
Watakabiliana wao kwa wao kuulizana.
Watasema: Kwa hakika nyinyi mlikuwa mkitujia upande wa kulia.
Watasema (wakubwa): Bali nyinyi wenyewe hamkuwa Waumini.
Sisi hatukuwa na mamlaka juu yenu, bali nyinyi wenyewe mlikuwa wapotovu.
Basi hukumu ya Mola wetu Mlezi imekwisha tuthibitikia. Hakika bila ya shaka tutaonja tu adhabu.
Tulikupotezeni kwa sababu sisi wenyewe tulikuwa wapotovu.
Basi wao kwa hakika siku hiyo watashirikiana katika adhabu pamoja.
Hivyo ndivyo tutakavyo wafanyia wakosefu.
Wao walipo kuwa wakiambiwa La ilaha illa 'Llahu Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu tu, wakijivuna.
Na wakisema: Hivyo sisi tuiache miungu yetu kwa ajili ya huyu mtunga mashairi mwendawazimu?
Bali huyu amekuja kwa Haki, na amewasadikisha Mitume.
Hakika nyinyi bila ya shaka mtaionja adhabu chungu.
Wala hamlipwi ila hayo mliyo kuwa mkiyafanya.
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
Hao ndio watakao pata riziki maalumu,
Matunda, nao watahishimiwa.
Katika Bustani za neema.
Wako juu ya viti wamekabiliana.
Wanazungushiwa kikombe chenye kinywaji cha chemchem
Kinywaji cheupe, kitamu kwa wanywao.
Hakina madhara, wala hakiwaleweshi.
Na watakuwa nao wanawake wenye macho ya staha mazuri.
Hao wanawake kama mayai yaliyo hifadhika.
Waingie kuulizana wenyewe kwa wenyewe.
Aseme msemaji mmoja miongoni mwao: Hakika mimi nalikuwa na rafiki
Aliye kuwa akinambia: Hivyo wewe ni katika wanao sadiki
Ati tukisha kufa tukawa udongo na mafupa, ndio tutalipwa na kuhisabiwa?
Atasema: Je! Nyie mnawaona?
Basi atachungulia amwone katikati ya Jahannamu.
Atasema: Wallahi! Ulikaribia kunipoteza.
Na lau kuwa si neema ya Mola wangu Mlezi bila ya shaka ningeli kuwa miongoni mwa walio hudhurishwa.
Je! Sisi hatutakufa,
Isipo kuwa kifo chetu cha kwanza? Wala sisi hatutaadhibiwa.
Hakika huku bila ya shaka ndiko kufuzu kukubwa.
Kwa mfano wa haya nawatende watendao.
Je! Kukaribishwa hivi si ndio bora, au mti wa Zaqqum?
Hakika Sisi tumeufanya huo kuwa ni mateso kwa walio dhulumu.
Hakika huo ni mti unao toka katikati ya Jahannamu.
Mashada ya matunda yake kama kwamba vichwa vya mashet'ani.
Basi hakika bila ya shaka hao watayala hayo, na wajaze matumbo.
Kisha juu yake wanyweshwe mchanganyo wa maji yamoto yaliyo chemka.
Kisha hakika marejeo yao bila ya shaka yatakuwa kwenye Jahannamu.
Hakika waliwakuta baba zao wamepotea.
Na wao wakafanya haraka kufuata nyayo zao.
Na bila ya shaka walikwisha potea kabla yao wengi wa watu wa zamani.
Na Sisi hakika tuliwapelekea waonyaji.
Basi hebu angalia ulikuwaje mwisho wa walio onywa.
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio khitariwa.
Na hakika Nuhu alitwita, na Sisi ni bora wa waitikiaji.
Na tulimwokoa yeye na ahali zake kutokana na msiba mkubwa.
Na tuliwajaalia dhuriya zake ndio wenye kubakia.
Na tukamwachia (sifa njema) kwa walio kuja baadaye.
Iwe salama kwa Nuhu ulimwenguni kote!
Kwa hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
Kisha tukawazamisha wale wengine.
Na hakika Ibrahim alikuwa katika kundi lake,
Alipo mjia Mola wake Mlezi kwa moyo mzima.
Alimwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?
Kwa kuzua tu mnataka miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu?
Mnamdhania nini Mola Mlezi wa walimwengu wote?
Kisha akapiga jicho kutazama nyota.
Akasema: Hakika mimi ni mgonjwa!
Nao wakamwacha, wakampa kisogo.
Basi akaiendea miungu yao kwa siri, akaiambia: Mbona hamli?
Mna nini hata hamsemi?
Kisha akaigeukia kuipiga kwa mkono wa kulia.
Basi wakamjia upesi upesi.
Akasema: Hivyo mnaviabudu vitu mnavyo vichonga wenyewe?
Na hali Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuumbeni nyinyi na hivyo mnavyo vifanya!
Wakasema: Mjengeeni jengo, na kisha mtupeni motoni humo!
Basi walitaka kumfanyia vitimbi, lakini tukawafanya wao ndio wa chini.
Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi; Yeye ataniongoa.
Ewe Mola wangu Mlezi! Nitunukie aliye miongoni mwa watenda mema.
Basi tukambashiria mwana aliye mpole.
فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَى فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَى قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ↓
Basi alipo fika makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye, alimwambia: Ewe mwanangu! Hakika mimi nimeona usingizini kuwa ninakuchinja. Basi angalia wewe, waonaje? Akasema: Ewe baba yangu! Tenda unavyo amrishwa, utanikuta mimi, Inshallah, katika wanao subiri.
Basi wote wawili walipo jisalimisha, na akamlaza juu ya kipaji.
Tulimwita: Ewe Ibrahim!
Umekwisha itimiliza ndoto. Hakika hivi ndivyo tunavyo walipa wanao tenda mema.
Hakika haya ni majaribio yaliyo dhaahiri.
Basi tukamtolea fidia kwa dhabihu mtukufu.
Na tukamwachia (sifa njema) kwa watu walio kuja baadaye.
Iwe salama kwa Ibrahim!
Hivi ndivyo tunavyo walipa wanao fanya mema.
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
Na tukambashiria kuzaliwa Is-haqa, naye ni Nabii miongoni mwa watu wema.
وَبَارَكْنَا عَلَيْهِ وَعَلَى إِسْحَاقَ وَمِن ذُرِّيَّتِهِمَا مُحْسِنٌ وَظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ مُبِينٌ ↓
Na tukambarikia yeye na Is-haqa. Na miongoni mwa dhuriya zao walitokea wema na wenye kudhulumu nafsi zao waziwazi.
Na kwa hakika tuliwafanyia hisani Musa na Haruni.
Na tukawaokoa wao na watu wao kutokana na dhiki kubwa.
Na tukawanusuru; na wakawa wao ndio wenye kushinda.
Na tukawapa wawili hao Kitabu kinacho bainisha.
Na tukawaongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
Na tukawaachia (sifa njema) katika watu walio kuja baadaye.
Iwe salama kwa Musa na Haruni!
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
Hakika wawili hao ni katika waja wetu walio amini.
Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.
Alipo waambia watu wake: Hamwogopi?
Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,
Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani?
Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa;
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye.
Iwe salama kwa Ilyas.
Hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa walio wema.
Hakika yeye ni katika waja wetu walio amini.
Na hakika Lut'i bila ya shaka ni miongoni mwa Mitume.
Tulipo mwokoa yeye na ahali zake wote,
Isipo kuwa mwanamke mkongwe katika wale walio bakia nyuma.
Kisha tukawaangamiza wale wengineo.
Na hakika nyinyi mnawapitia wakati wa asubuhi,
Na usiku. Basi je! Hamyatii akilini?
Na hakika Yunus alikuwa miongoni mwa Mitume.
Alipo kimbia katika jahazi lilio sheheni.
Akaingia katika kupigiwa kura, na akawa katika walio shindwa.
Samaki akammeza hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa.
Na ingeli kuwa hakuwa katika wanao mtakasa Mwenyezi Mungu,
Bila ya shaka angeli kaa ndani yake mpaka siku ya kufufuliwa.
Lakini tulimtupa ufukweni patupu, hali yu mgonjwa.
Na tukauotesha juu yake mmea wa kabila ya mung'unye.
Na tulimtuma kwa watu laki moja au zaidi.
Basi wakaamini, na tukawastarehesha kwa muda.
Basi waulize: Ati Mola wako Mlezi ndiye mwenye watoto wa kike, na wao wanao watoto wa kiume?
Au tumewaumba Malaika kuwa ni wanawake, na wao wakashuhudia?
Ati ni kwa uzushi wao ndio wanasema:
Mwenyezi Mungu amezaa! Ama hakika bila ya shaka hao ni waongo!
Ati amekhiari watoto wa kike kuliko wanaume?
Mna nini? Mnahukumu vipi nyinyi?
Hamkumbuki?
Au mnayo hoja iliyo wazi?
Basi leteni Kitabu chenu kama mnasema kweli.
وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ ↓
Na wameweka makhusiano ya nasaba baina yake na majini; na majini wamekwisha jua bila ya shaka kuwa wao watahudhurishwa.
Subhana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo msingizia.
Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa.
Basi hakika nyinyi na mnao waabudu
Hamwezi kuwapoteza
Isipo kuwa yule atakaye ingia Motoni.
Na hapana katika sisi ila anapo mahali pake maalumu.
Na hakika bila ya shaka sisi ndio wajipangao safu.
Na hakika sisi ndio wenye kusabihi kutakasa.
Na walikuwapo walio kuwa wakisema:
Tungeli kuwa na Ukumbusho kama wa watu wa zamani,
Bila ya shaka tungeli kuwa ni waja wa Mwenyezi Mungu wenye ikhlasi.
Lakini waliukataa. Basi watakuja jua.
Na bila ya shaka neno letu lilikwisha tangulia kwa waja wetu walio tumwa.
Ya kuwa wao bila ya shaka ndio watakao nusuriwa.
Na kwamba jeshi letu ndilo litakalo shinda.
Basi waachilie mbali kwa muda.
Na watazame, nao wataona.
Je! Wanaihimiza adhabu yetu?
Basi itakapo shuka uwanjani kwao, itakuwa asubuhi mbaya kwa walio onywa.
Na waache kwa muda.
Na tazama, na wao wataona.
Subhana Rabbi'l'Izzat Ametakasika Mola Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia.
Na Salamu juu ya Mitume.
Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.